HTML Tables
Elimu

WANANCHI WANAOSTAHILI PASI YA KUSAFIRIA YA KIDIPLOMASIA TANZANIA

Pasi ya kusafiria yenye hadhi ya kidiplomasia ni pasi anayopewa mtu anayetakiwa kusafiri kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kazi za Kuiwakilisha nchi. Pasi hizi wanapewa watu wenye hadhi ya kidiplomasia tu wanaopangiwa vituo vya kazi nje ya nchi na pia kwa baadhi ya watumishi wa Serikali. Pasi hizi zinakuwa na rangi tofauti na pasi za kawaida na kuzifanya zitambulike kirahisi. Kwenye nchi nyingi ikiwamo Tanzania, ganda la nje la pasi hii ni jeusi – si la rangi ya kijani kama zilivyo pasi nyingine. Kuwa na pasi ya kidiplomasia haimaanishi mtu huyo ana kinga ya kidiplomasia.

 

Pasi ya kusafiri yenye hadhi ya kidiplomasia inaweza kutolewa kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ana haki ya kupewa pasi ya aina hiyo kama ilivyoelezwa kwenye Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Pasi na Nyaraka za Kusafiria ya mwaka 2002.

 

Wenye haki ya kupewa pasi ya kidiplomasia ya Tanzania

Wafuatao ni watu wenye haki ya kupatiwa pasi ya kusafiria ya kidiplomasia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania:

 

Kutoka Serikali Kuu , wanaostahili kupewa pasi hizi ni: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Mawaziri na Manaibu Waziri.

 

Kutoka kwenye mhimili wa Bunge, wanaostahili ni: Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi pamoja na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi.

 

Kutoka kwenye mhimili wa Mahakama, wanaostahili pasi hii ni: Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jaji wa Mahakama Kuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 

Wamo pia mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania kwenye nchi mbalimbali, Katibu Mkuu, Katibu Mkuu Kiongozi na Naibu Katibu Mkuu Kiongozi pamoja na Makatibu wa Bunge.

 

Kutoka kwenye vyombo vya Ulinzi na Usalama wa nchi , wanaostahili kupatiwa pasi hii ni: Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (CDF), Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wenye/kuzidi cheo cha Meja Jenerali wa Jeshi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Makamishna wa Jeshi la Polisi, Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini na Makamishna wa Jeshi la Magereza.

 

Kutoka Benki Kuu ya Tanzania , wanaostahili pasi hii ni Gavana na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

 

Wengine ni Makatibu (wasaidizi) wa viongozi wafuatao: Katibu wa Rais, Katibu wa Makamu wa Rais, Katibu wa Rais wa Zanzibar, Katibu wa Waziri Mkuu na Katibu wa Waziri Kiongozi.

 

Pia wamo Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwenyekiti wa Tume yoyote ya Serikali, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB), Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji na Mtumishi wa Serikali anayefanya kazi nje ya nchi .

 

Wengine wanaostahili kuwa na pasi hii kutokana na nafasi za uongozi walizowahi kuwa nazo nchini ambao wameshastaafu kwenye nafasi hizo ni:

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu, Waziri Kiongozi, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi, Naibu Spika, Jaji Mkuu, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Jaji wa Mahakama Kuu.

 

Pia, wapo waliostaafu kwenye nafasi za Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Makamishna wa Jeshi la Polisi, Kamishna wa Jeshi la Magereza, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) na Wakuu wa Taasisi za Kidini endapo Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji ataona inafaa wapewe.

 

Watu wenye pasi ya kusafiria ya kidiplomasia lazima watambuliwe/kutambulishwa kwa uongozi wa nchi wanazokwenda kama mmoja wa timu ya wanadiplomasia kabla hajapewa haki ya kupatiwa stahiki zake za kidiplomasia.

Uongozi wa nchi husika unatakiwa kuhakikisha kuwa watu waliopewa pasi ya aina hii wanakuwa huru kusafiri ndani ya nchi yao bila kuzuiwa.

 

Pasi za kidiplomasia zinaweza kufutwa na Serikali bila mmiliki kupewa taarifa yoyote iwapo pasi hiyo itatumiwa tofauti na masharti ya matumizi yake kama yalivyoelezwa wakati wa kupatiwa pasi hiyo.

 

Kama mtu akiwa ana haki ya kupewa pasi ya aina hii, moja kwa moja familia yake (mke/mume na watoto) wanakuwa wamefuzu kupewa pasi hii pia. Baada ya kupatiwa pasi ya aina hii, kinachotakiwa ni kuomba visa ya kidiplomasia unaposafiri ingawa kuna baadhi ya nchi zinaruhusu kuingia bila visa unapokuwa na pasi hii

 

Pasi hii inaweza kutumika kwenye majukumu ya kitaifa. Kama atasafiri kama mtalii, anatakiwa kubeba pasi yake ya kawaida kama mtu mwingine yoyote. Baadhi ya wenye pasi hii hubeba pasi zote mbili kwa wakati mmoja, kwa mfano kama mtu amepangiwa kwenda Uingereza kwa shughuli maalum lakini akaamua kupitia Uarabuni kwanza kama mtalii, ni muhimu kwake pasi zote mbili zigongwe mihuri anapotoka na kuingia nchi nyingine.

 

Hairuhusiwi kuingia kwenye nchi nyingine kutumia pasi moja na kutoka na pasi nyingine.

 

Baadhi ya kampuni na watu binafsi wanadai wanaweza kukusaidia kupata pasi za kidiplomasia pamoja na kinga ya kidiplomasia kwa gharama fulani. Watu au kampuni hizi ni za kitapeli kwakuwa mtu utakuwa na hadhi ya kupewa pasi hii ukiwa na shughuli ya kuiwakilisha nchi tu, na wanaostahili kuwa na pasi hii wanapewa taarifa za jinsi ya kuiomba wanapokuwa na safari ya nje ya nchi.

2 Comments

2 Comments

  1. Pingback: creditmattersinc.org

  2. Pingback: Mari Gartrell

You must be logged in to post a comment Login

Leave a Reply

To Top