HTML Tables
Michezo

SIMBA SC KUINGIA VITANI KUISAKA NDANDA FC

Vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC wanatarajiwa kuanza safari mjini Dar es Salaam kwenda Mtwara kwa ajili ya mchezo dhidi ya Ndanda FC Jumamosi Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

 
Wachezaji wote wanatarajiwa kuwa safarini kesho kwa ajili ya mchezo huo, ukiondoa kipa Said Mohammed ‘Nduda’ na mabeki Shomary Kapombe na Salim Mbonde ambao ni majeruhi.
Simba ipo kambini katika hoteli ya SeaScape, Kunduchi mjini Dar es Salaam tangu jana baada ya mapumziko ya siku mbili kwa ajili ya sikukuu ya Krisimasi.
Simba SC wataondoka kesho wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kuvuliwa mapema ubingwa wa Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kuchapwa kwa penalti 4-3 na Green Warriors ya Mwenge kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.

 
Lakini wanakwenda Mtwara wakiwa wanaongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 23 sawa na Azam FC, wakiwazidi kwa pointi mbili mabingwa watetezi, Yanga SC baada ya timu zote kucheza mechi 11.

Kwa ujumla, Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea Ijumaa baada ya mapumziko ya wiki tatu kupisha michuano ya CECAFA Challenge iliyomalizika nchini Kenya wiki iliyopita kwa wenyeji, Harambee Stars kuwa mabingwa wakiwafunga Zanzibar katika fainali.

Click to comment

You must be logged in to post a comment Login

Leave a Reply

To Top