HTML Tables
Michezo

SIMBA NA YANGA ZAPEWA ONYO KALI

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amezitaka klabu za Ligi Kuu Tanzania kuhakikisha zinakuwa na viwanja vyao vya mazoezi na mashindano vinginevyo zinaweza kukosa sifa ya kushiriki michuano ya kimataifa.
Aidha, Karia alisema pamoja na mkakati huo ambao ni agizo la Shirikisho la Soka duniani (Fifa), TFF haitakubali ubabaishaji unaofanywa na klabu za Ligi Kuu kuhusu agizo la kuwa na timu za vijana za madaraja tofauti.

Karia alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa TFF na wahariri wa vyombo vya habari nchini uliofanyika jana katika Hoteli ya Sea Scape jijini Dar es Salaam kwa lengo la kueleza walichokifanya kwa kipindi cha miezi minne tangu walivyoingia madarakani na mikakati yao ya mbeleni.

Hata hivyo, rais huyo wa TFF alilazimika kutoa ufafanuzi huo wakati alipoulizwa kuhusu maendeleo ya timu ya vijana inayoandaliwa kwa ajili ya michuano ya Caf ya U-17 inayotarajiwa kufanyika nchini mwaka 2019.

“Fifa haitaki ubabaishaji, hata sisi (TFF), imetuambia haitatueleza ni lini inakuja kufanya ukaguzi wa mahesabu yetu, itakuja kwa kushtukiza, hivyo kuna uwezekano ipo siku klabu zetu zikazuiwa kushiriki michuano ya kimataifa kama hazitazingatia kuwa na viwanja vyao vya mazoezi na mechi,” alisema na kuongeza.

“Pia kuanzia sasa na sisi hatutakubali ubabaishaji kwa klabu ambazo zinaokoteza timu za vijana, tunataka kila klabu iwe na timu za madaraja tofauti ya timu za vijana, vinginevyo kuanzia msimu ujao hatutaziruhusu kushiriki Ligi Kuu.”

Agizo hilo la viwanja ni msumari wa moto zaidi kwa klabu kongwe Simba na Yanga zinazodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, ambazo mara nyingi zimekuwa zikiiwakilisha Tanzania Bara kwenye michuno ya kimataifa, huku zikiwa hazina hata uwanja wa mazoezi.

Azam ambayo nayo imekuwa ikiiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa, licha ya uchanga wake Ligi Kuu Bara ukilinganisha na wakongwe hao, yenyewe imekidhi vigezo hivyo kutokana na kuwa na viwanja vyake ambavyo vinakubalika na Fifa.

Akizungumzia baadhi ya mambo ambayo wameyafanikisha kwa maendeleo ya soka la Tanzania, Karia alisema ni pamoja na kutatua tatizo la ulipaji kodi TRA pamoja na makato ya mifuko ya jamii lililokuwa likiikabili TFF.

Karia pia alisema kutokana na uwezo mdogo kifedha unaolikabili shirikisho hilo, hawataweza kujenga shule za kulea vipaji, lakini mkakati wao wa kukuza vipaji, wameanza kwa kutumia mashindano ya shule za msingi na sekondari kupitia Wizara ya Tamisemi.

Kadhalika, Karia alitolea ufafanuzi kuhusu kituo cha michezo kinachojengwa Tanga kwa kufafanua kuwa ujenzi huo ni kama ulivyo ule wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

“Tutakaa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (Paul Makonda), ili kuangalia uwezekano wa kupata eneo kwa ajili ya kituo kingine kama hiki cha Karume, lakini ujenzi huo hautakuwa Ilala ama Temeke,” alisema.Aidha, Karia amefuta mashindano yoyote ya soka yaliyo nje ya mfumo wa TFF isipokuwa tu kwa kibali maalum.

Alisema mashindano ya soka yasiyo rasmi kama yale yanayoandaliwa na wanasiasa majimboni na hata na baadhi ya taasisi na wadau, sasa yanapswa kuandaliwa kwa mujibu wa kanuni za TFF kupitia wawakilishi wao eneo husika.

Karia alisema wakati umefika sasa wabunge na wanasiasa kwa ujumla kutoa fedha kuzidhamini timu za majimboni mwao badala ya kuanzisha mashindano ya ng’ombe na mbuzi.

Click to comment

You must be logged in to post a comment Login

Leave a Reply

To Top