HTML Tables
Habari

SERIKALI YAUFUNGUA MGODI WA BUHEMBA

Hatimaye Serikali imefungua Migodi ya Dhahabu ya Wachimbaji Wadogo iliyopo katika eneo la Buhemba Wilaya ya Butiama Mkoani Mara baada ya kujiridhisha hali ya usalama katika migodi hiyo.

Migodi hiyo imefunguliwa rasmi na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na kushuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi.

Akizungumza katika tukio hilo, Nyongo alisema eneo la Buhemba lina jumla ya migodi ya dhahabu 16 ambayo inamilikiwa na wachimbaji wadogo hata hivyo iliyokidhi vigezo vya kiusalama ni migodi 10 pekee ambayo imeruhusiwa kuendeleza shughuli za uchimbaji.

Aidha Nyongo aliagiza wakaguzi wa migodi kuhakikisha wanatembelea mara kwa mara maeneo ya migodi ili kukagua hali ya usalama pamoja na kutoa mafunzo ya uchimbaji salama kwa wachimbaji hususani wadogo lengo likiwa ni kuepusha ajali.

Pia aliwataka wachimbaji madini kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na taratibu za uchimbaji ili kuepusha ajali migodini na wakati huohuo kunufaika ipasavyo na shughuli zao bila kupata usumbufu na kalipa kodi na tozo mbalimbali kwa mujibu wa sheria na alionya kwamba mgodi utakaoshindwa kulipa inavyostahili, utafungiwa.

Serikali ilisitisha shughuli za uchimbaji Madini kwenye eneo hilo la Buhemba Februari 2017 baada ya kutokea vifo vya wachimbaji saba na wengine wapatao 15 kujeruhiwa kutokana na kufanya shughuli zao bila kuzingatia taratibu na kanuni za uchimbaji salama.

Click to comment

You must be logged in to post a comment Login

Leave a Reply

To Top