HTML Tables
Habari

KIWANDA CHA SUKARI NA POLISI LAWAMANI KWA KULAZUMISHA WAFANYAKAZI KUANDIKA BARUA ZA KUACHA KAZI

Kiwanda cha sukari Mtibwa kilichopo wilayani Mvomero kimadaiwa kiwafukuza kazi wafanyakazi saba kwa kuwalazimisha kuandika barua za kuacha kazi wakiwa chini ya ulinzi wa polisi.

 

Wafanyakazi hao imedaiwa wamelazimishwa kufanya hivyo kwa tuhuma za kuandaa mgomo wa kushinikiza nyongeza ya mshahara.

 

Hata hivyo kiwanda hicho kimekanusha kufanya hivyo kwa wafanyakazi hao.

 

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi akizungumza kwa njia ya simu mmoja wa wafanyakazi aliyekumbwa na kadhia hiyo, Sudy Ntutuguru amesema Septemba 26 mwaka huu walikuwa wamekubaliana kuwa na mkutano na mwajiri kwaajili ya kujadili suala la nyongeza ya asilimia kumi ya mshahara.

 

Nyongeza hiyo ni kwa mujibu wa mkataba wa hali bora ya kazi namba 10 ambayo walitarajia kuipata tangu Agosti lakini hawakuipata.

 

“Tukiwa tunasubiri kuonana na mwajiri tulitangaziwa kwamba tuendelee na kazi kwani mwajiri hawezi kukutana na sisi siku hiyo lakini tulisema hatuwezi kuendelea na kazi hadi tujue hatma yetu,” amesema Ntutuguru.

 

Amesema wakati Uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani na Viwandani (TPAWU) kiwandani hapo ukiendelea kuomba uongozi kuzungumza kwanza na wafanyakazi ndipo yalipofika magari mawili ya polisi ya FFU na gari la maji ya kuwasha na mabasi matatu ambapo tuliagizwa kwenda shambani ama kupanda mabasi kwaajili ya kurejea makwetu hivyo wafanyakazi wote wakaamua kwenda shambani.

 

Amesema baada ya wenzao kurejea shambani yeye na wenzie sita walikamatwa na polisi.

 

“Tulipelekwa katika kituo cha polisi kilichopo kiwandani na kuhojiwa kwa siku mbili na kesho yake tukiwa polisi tuliletewa karatasi na kulazimishwa kuandika barua za kuacha kazi chini ya ulinzi wa polisi na tulipokamilisha tulichukuliwa na kurejeshwa kambini,”

 

“Tulisimamiwa na polisi kukusanya kila kilicho chetu na kisha kupakiwa kwenye magari na kupelekwa hadi kituo kikuu cha mabasi Msamvu ambako tulipakiwa kwenye mabasi ili kurejea makwetu mimi kwa sasa nipo Dar,” amesema Ntutuguru lakini polisi wameeleza kuwa jambo hilo halina ukweli wowote.

 

Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, meneja mkuu wa kiwanda hicho, Stanley Rau alikiri kwamba kulitokea kutokuelewana katika baadhi ya vipengele vya makubaliano ya kazi lakini tayari walisharekebisha tatizo hilo.

 

Hata hivyo meneja huyo alikanusha suala la wafanyakazi kulazimishwa kuandika barua za kuacha kazi chini ya ulinzi wa polisi na kwamba walioacha kazi waliamua wenyewe.

 

Kwa upande wake ofisa utumishi wa kiwanda hicho, Ezekiel Masinde alikataa kabisa kuzungumzia suala la wafanyakazi hao kulazimishwa kuacha kazi kwa madai kuwa mwajiri namba moja ni meneja mkuu na ndiye anayepaswa kutolea ufafanuzi suala hilo.

 

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leons Rwegasira amesema siku ya tukio walipigiwa simu na uongozi wa kiwanda na kutaarifiwa kuwa wakata miwa wamegoma hivyo wanahitaji msaada wa polisi.

 

“Kazi yetu ni kulinda amani hivyo tulipopokea taarifa hizi tulituma askari wetu kwenda kuimarisha ulinzi kiwandani hapo, japo tuna kituo cha polisi pale tuliamua kuongeza nguvu maana tuliarifiwa hali sio shwari,” amesema.

 

Kuhusu suala la askari kushiriki kuwalazimisha wafanyakazi kuandika barua za kuacha kazi kamanda huyo alikanusha kwa akieleza kuwa suala la kuacha kazi ni la mwajiri na mwajiriwa.

 

Kamanda Rwegasira amesema suala la askari kuwasindikiza hadi kituo kikuu cha mabasi Msamvu na kuwapakiwa kwenye mabasi wafanyakazi walioondolewa halina ukweli wowote.

 

Kiwanda cha Sukari Mtibwa kinakadiriwa kuwa na wafanyakazi zaidi ya 2,500 huku wa mashambani ambao ndio walioendesha mgomo wakiwa takriban 600.

 

Akizungumzia mgogoro huo, Katibu wa TPAWU Mkoa wa Morogoro, Nicholaus Ngowi amesema uliotokea kiwandani hapo kulitokana na mwajiri kushindwa kutekeleza makubaliano yaliyo katika mkataba wa kazi na mkataba wa hali bora namba 10 uliosainiwa na pande zote mbili Julai 31 mwaka huu.

 

Click to comment

You must be logged in to post a comment Login

Leave a Reply

To Top